Picha na mtandao
Kikosi cha vinara wa Ligi Kuu Bara
kinaendelea kujifua vilivyo kisiwani Unguja kwa ajili ya mchezo wake wa
Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga utakaofanyika Jumamosi ijayo kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani
mkubwa kutokana na vita iliyopo kati ya timu hizo ya kuwania ubingwa wa
ligi kuu msimu huu ambapo mpaka sasa Simba ndiyo ipo kileleni ikiwa na
pointi 51 wakati Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 49.
Hata hivyo, ili kuhakikisha Simba
inaibuka na ushindi katika mchezo huo, kocha mkuu wa timu hiyo,
Mcameroon, Joseph Omog amemtengea dakika 30 za mazoezi ya kufunga kila
siku, mshambuliaji wake raia wa Burundi, Laudit Mavugo ili aiangamize
Yanga.
Katika mazoezi ya timu hiyo huko Unguja,
Omog amekuwa akimfua Mavugo pamoja na washambuliaji wengine wa timu
hiyo kwa dakika 30 kila siku akiwapatia mbinu mbalimbali za kuzifumania
nyavu kabla ya kuanza mazoezi ya pamoja na kikosi kizima.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Omog
alisema kuwa amekuwa akifurahishwa na jinsi Mavugo anavyofanya vizuri
katika mazoezi hayo lakini pia wachezaji wengine, hivyo anaamini
atafanya vizuri dhidi ya Yanga.
“Tunaendelea vizuri na mazoezi yetu,
wachezaji wote tuliokuja nao huku wapo vizuri hata wale waliokuwa
majeruhi maendeleo yao siyo mabaya.
“Kuhusiana na Mavugo yupo vizuri
anaendelea kujifua vilivyo na kila siku anazidi kufanya vizuri mazoezini
kwa muda wote ambao nimekuwa nikiwafundisha, hivyo ni matumaini yangu
ataendeleza rekodi yake ya kuzifumania kama alivyofanya katika mechi
tatu zilizopita,” alisema Omog.
Simba ipo visiwani Zanzibar tangu Ijumaa iliyopita, hivyo leo wanafikisha siku ya nne visiwani humo.
CHANZO:SALEH JEMBE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni