rooney
Wayne Rooney.
henry
Thierry Henry.
Na Mwandishi wetu,
Nahodha wa Manchester United, Wayne Rooney amefanikiwa kuvunja rekodi iliyokuwa imewekwa na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry baada ya kuifungia klabu yake katika mchezo wa ligi kuu ya Uingereza dhidi ya Liverpool.
Rooney amevunja rekodi ya Henry ya kufunga magoli mengi kwenye michezo ya ligi kuu wa Uingereza kwa kuchezea timu moja ambapo Henry alikuwa na rekodi ya kufunga magoli 175 katika michezo 258 na aliyafunga kwa kipindi cha mwaka 1999-2007 na baadae kwa mkopo kwenye msimu wa 2011-2012.

Rooney yeye kafikisha magoli 176 akiwa na Manchester United pekee ambapo ameyafunga magoli hayo katika michezo 358 kwa kipindi cha misimu 12 huku Henry akitumia misimu 9 kuweka rekodi hiyo.
Hata hivyo licha ya Rooney kutumia michezo mingi kufikia rekodi hiyo lakini inaonekana magoli ya Rooney kuwa na msaada zaidi kwa klabu yake kwani kwa kipindi hicho cha misimu 12 ameisaidia klabu yake kutwaa mataji matano na Henry akipata mataji mawili.
Pamoja na kufikia rekodi hiyo lakini pia goli ambalo Rooney alifunga katika mchezo wa Liverpool amefikisha magoli 242 ambayo tayari ameifungia Manchester United kwa kipindi chote alichoichezea na kuwa amebakiza magoli saba kufikia rekodi ya Sir Bobby Charlton ya ufungaji magoli mengi wa muda wote katika klabu hiyo.
Pia goli hilo la Rooney dhidi ya Liverpool amefikisha michezo minne mfululizo akiifungia United kwa kuanzia mchezo wa Swansea, Sheffield United na Newcastle United ambapo mara ya mwisho alifanya hivyo March, 2012.