TANGAZO

TANGAZO

Jumatano, 27 Januari 2016

Vuta nikuvute bungeni, Chenge ahairisha kikao



Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge 
Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge amelazimika kuahirisha kikao cha Bunge mara mbili leo asubuhi baada ya wabunge wa upinzani kupinga hoja ya serikali ya kutorusha moja kwa moja shughuli zote za Bunge hicho kupitia TBC.
Vuta nikuvute hiyo ilitokana na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kutoa kauli ya serikali kuwa TBC itapunguza muda wa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kituo hicho cha luninga cha umma.
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) akiungwa mkono na wabunge wenzake kutoka kambi ya upinzani, alipinga hoja hiyo ya serikali na kumtaka Chenge asitishe mjadala wa hotuba ya Rais John Magufuli hadi hoja hiyo ya serikali itakapojadiliwa.
Zitto alisema TBC ni mali ya umma na inaendeshwa kwa kodi za wananchi ambao wana haki kuhabarishwa bila kuangalia gharama zinazotajwa na serikali kwani kituo hicho hakiendeshwi kibiashara.
Huku Chenge akijitahidi kumtuliza ili ratiba ya Bunge iendelee kama ilivyopangwa, Zitto aliungwa mkono na Halima Mdee, Mbunge wa Kawe (Chadema) hali iliyomfanya mwenyekiti huyo aliyechaguliwa jana kusema ataagiza Kamati ya Uongozi kujadili mara moja.
Kana kwamba hiyo haitoshi, wabunge wa upinzani walimjia juu Chenge kutaka Bunge lisiendelee kujadili hotuba ya Dk Magufuli iliyorushwa ‘live’ mwishoni mwa mwaka jana, mara baada ya kuapishwa kuwa rais wa nchi.
Baada ya malumbano yaliyoambatana na kurushina vijembe baina ya wabunge wa kambi ya upinzani na wale wa chama tawala, CCM, Chenge alisitisha kikao cha Bunge kwa saa moja kutafakari hoja hiyo.
Hata hivyo Chenge aliyesitisha kikao cha bunge kupisha Kamati ya Uongozi kukutana na kutoa mrejesho baada ya saa moja alilazimika kuahirisha tena Bunge hadi jioni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni