MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ameshinda
tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika katika sherehe zilizofanyika
usiku huu ukumbi wa mikutano wa Kimataifa mjini Abuja.
Samatta amepata pointi 127, mbele ya mchezaji mwenzake wa TP Mazembe,
kipa Robert Muteba Kidiaba wa DRC, aliyepata pointi 88, wakati
mshambuliaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia na timu ya taifa ya Algeria,
Baghdad Bounedjah amepata pointi 63.
Mafanikio ya Samatta anayeweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza
kushinda tuzo kubwa ya Afrika, yanakuja baada ya kuiwezesha Mazembe
kutwaa taji la tano la Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiibuka mfungaji
bora kwa mabao yake nane.
Mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa mara ya kwanza.
Mchezaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 26,
amewaangusha Yaya Toure wa Ivory Coast aliyekuwa anashikilia tuzo hiyo
na Andre Ayew wa Ghana.
Amekusanya pointi 143, saba zaidi ya Toure wakati Ayew ameshika nafasi
ya tatu kwa kupata pointi 112 na anakuwa mchezaji wa kwanza wa
Gabon kushinda tuzo ya CAF
Kiungo wa Nigeria, Etebo Peter Oghenekaro ameshinda tuzo ya Mchezaji
Anayechipukia Vizuri dhidi ya Mnigeria mwenzake, Azubuike Okechukwu,
kipa wa Mali, Djigui Diarra, Mahmoud Abdelmonem Abdelhamid ‘Kahraba’ wa
Misri na Mualgeria, Zinedine Ferhat.
Etebo, anayechezea timu ya Ligi Kuu ya Nigeria, Warri Wolves, aling’ara
katika michuano ya U-23 ya Afrika Desemba nchini Senegal, akiibuka
mfungaji bora kwa mabao yake matano, yakiwemo mawili aliyofunga katika
ushindi wa 2-1 dhidi ya Algeria katika fainali.
Mshambuliaji kinda wa Nigeria, Victor Osimhen ameshinda tuzo ya
Mwanasoka Bora Chipukizi akimshinda ndugu yake, Kelechi Nwakali,
wachezaji wawili wa Mali, Adama Traore na Samuel Diarra na Yaw Yeboah wa
Ghana.
Osimhen anayeshinda tuzo hiyo siku tisa tangu asherehekee kufikisha
miaka 17 ya kuzaliwa, mafanikio hayo yanafuatia kufanya kwake vizuri
katika Kombe la Dunia la U-17 Oktoba mwaka jana nchini Chile, akifunga
mabao 10 na kuibuka mfungaji bora sambamba na kushinda Mpira wa Fedha
baada ya Mchezaji Bora wa pili wa michuano hiyo, huku Nigeria ikitwaa
Kombe.
Anakuwa mchezaji wa pili wa Nigeria kushinda tuzo hiyo baada ya Kelechi Iheanacho mwaka jana.
Mfaransa, Herve Renard ameshinda tuzo ya kocha bora wa mwaka kwa mara ya
pili, baada ya kuipa Ivory Coast ubingwa wa Afrika mwaka jana nchini
Equatorial Guinea.
Mfaransa huyo amewashinda Baye Ba wa Mali U-17, Patrice Carteron wa TP
Mazembe, Faouzi Benzarti wa Etoile du Sahel na Emmanuel Amunike wa
Nigeria U-17.
Samatta akiwa na Aubameyang katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa Abuja kabla ya kutangazwa washindi
Renard, ambaye alishinda tuzo ya kwanza baada ya kuipa Zambia ubingwa wa
Afrika mwaka 2012, alikabidhiwa tuzo yake na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya CAF, Adoum Djibrine.
Cameroon imezishinda Ghana, Afrika Kusini na Zimbabwe katika kipengele
cha timu bora ya taifa ya wanawake, wakati Ivory Coast imeziangusha
Ghana, Mali U-17, Nigeria U-17 na Nigeria U-23 katika timu bora ya taifa ya wanaume.
Refa wa Gambia, Papa Bakary Gassama ameshinda tuzo ya refa bora kwa mara
ya pili mfululizo akiwaangusha Ghead Zaglol Grisha wa Misri, Janny
Sikazwe wa Zambia na Eric Arnaud Otogo Castane wa Gabon.
Mualgeria, Haimoudi Djamel pia alishinda tuzo hiyo mara mbili mfululizo mwaka 2012 na 2013.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni