TANGAZO

TANGAZO

Jumatatu, 4 Januari 2016

NANI NI NANI SERIKALI YA JPM?: Dk Hussein Mwinyi – Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Dk Hussein Mwinyi ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi

Historia na Elimu
Dk Hussein Mwinyi ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli. Kiongozi huyu pia ni mbunge wa jimbo la Kwahani lililoko Unguja, Zanzibar.
Dk Hussein Mwinyi ana miaka 49 hivi sasa na
ifikapo Desemba 2016 atatimiza miaka 50. Alizaliwa Desemba 23, 1966 kwenye kisiwa cha Unguja, Zanzibar. Dk Mwinyi ni mtoto wa Mzee Ali Hassan Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na mama Sitti Mwinyi ambaye amekuwa (First Lady) katika awamu ya pili.
Kwa sababu ya kazi za baba yake mzazi, Dk Mwinyi alianza elimu ya Msingi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 – 1976 akisoma katika Shule ya Msingi Oysterbay. Mwaka 1984 hadi 1985 wazazi wake walimhamishia Misri ambako aliendelea na masomo ya elimu ya msingi hadi kuhitimu katika Shule ya Msingi “Manor House Junior”. Shule hii ilikuwa na hadhi ya “Middle School za Tanzania” kwa wakati huo. Hussein Mwinyi alipelekwa Misri kwa sababu baba yake (Ali Hassan Mwinyi) alihamishiwa nchini Misri kikazi kama balozi wa Tanzania nchini Misri wakati huo.
Hussein Mwinyi alirejea Tanzania na kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Azania ambako alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne mwaka 1982 – 1984. Alipohitimu kidato cha nne alifaulu na kupangiwa Shule ya Sekondari Tambaza kusoma kidato cha tano na cha sita, hata hivyo aliishia kusoma kidato cha tano peke yake mwaka 1984/1985, mwaka huo huo 1985 alienda nchini Uturuki kusomea utabibu wa binadamu. Alianza masomo ya udaktari nchini Uturuki mwaka 1985 kwenye Shule ya Utabibu ya Chuo Kikuu cha Marmara na kuhitimu Shahada ya Utabibu wa Binadamu mwaka 1992.
Kwa sababu hakumaliza kidato cha sita, alipokuwa huko ughaibuni alipitia masomo ya mwaka mmoja ya kujiandaa na udahili wa Chuo Kikuu “Pre University Studies”. Wakti huo Chuo cha Marmara kilikuwa kinapokea hata wanafunzi wa kidato cha nne kuanza kusomea shahada ya utabibu, lakini lazima wapitie mwaka mmoja wa maandalizi kama alivyofanya Mwinyi. (Sikufanikiwa kupata mawasiliano na chuo hiki ili kujiridhisha ikiwa hadi sasa wanatumia utaratibu huo)
Mwaka 1993, Mwinyi alikwenda nchini Uingereza kujiendeleza zaidi kielimu, aliendelea na masomo ya juu ya utabibu katika Hospitali ya Hammersmith ambako alihitimu shahada ya uzamili ya utabibu mwaka 1994 na kuunganisha shahada ya uzamivu ya udaktari hapohapo Hammersmith ambayo aliihitimu mwaka 1997.
Dk Mwinyi amemuoa Mariam Herman na wana watoto wanne; Ibrahim, Jamila, Tariq na Sitti.
Uzoefu
Dk Mwinyi hakuishia tu kuwa daktari wa mdomoni, amefanya kazi za kidaktari. Alipohitimu shahada ya kwanza ya utabibu alirejea Tanzania na kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Na hata baada ya ya kuhitimu shahada ya uzamivu nchini Uingereza, alirejea nchini kwa mara nyingine na kufanya kazi katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Herbert Kairuki (HKMU) kwa miaka miwili hadi mwaka 1999.
Kiongozi huyu alijitosa kwenye siasa mwaka 1999 akiliwania Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani (Bara) na kushinda. Alipokuwa mbunge, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alikaa katika wadhifa huo hadi mwaka 2005.
Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 Dk Mwinyi alijitosa tena jimboni, lakini safari hii siyo Mkuranga. Ilikuwa ni jimbo la Kwahani, Zanzibar – ambako alipambana na kuwashinda wagombea sita kutoka vyama vingine akipata kura 6,239 sawa na asilimia 85.6 akifuatiwa na Mussa Haji Khamis wa CUF aliyeambulia kura 921 sawa na asilimia 12.6. Baada ya kuwa mbunge kwa mara ya pili, Serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Jakaya Kikwete na Dk Mwinyi ilimteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais na alidumu hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikokaa hadi mwaka 2010.
Mwinyi alirejea tena na kugombea ubunge katika jimbo la Kwahani mwaka 2010, akashindana na yuleyule hasimu wake wa mwaka 2005, Haji wa CUF, mara hii vyama vingine havikuweka wagombea na Dk Mwinyi hakupata shida kushinda kwa kura 5,277 sawa na asilimia 83.0 dhidi ya kura 1,085 sawa na asilimia 17.0 za CUF. Mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 Rais Kikwete akamteua Mwinyi kuwa Waziri wa Ulinzi kabla ya kumrejesha Wizara ya Afya mwaka 2012 na miezi 19 baadaye (yaani Januari, 2014) kwa mara nyingine tena akamteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, nafasi aliyodumu hadi mwaka 2015.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Dk Mwinyi alirudi tena katika jimbo la Kwahani, hii ikiwa ni mara ya nne akisaka nafasi ya kuwawakilisha wananchi, akafanikiwa kumshinda Khalid Rajab Mgana wa CUF na kuchaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha nne. Rais JPM amemteua Mwinyi kuwa Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa na hivyo kumuongezea rekodi ya kuongoza wizara hiyo kwa kitambo cha kutosha.
Mwaka 2015 Dk Mwinyi alitajwa sana kama mmoja wa wanasiasa wanaoweza kuvaa viatu vya JK ikiwa CCM ingeamua mrithi huyo atokee upande wa Zanzibar, hata hivyo yeye mwenyewe hakuwa na nia na hakuchukua hata fomu kwa ajili ya kuwania kiti hicho.
Ndani ya CCM Dk Mwinyi anashikilia nyadhifa mbalimbali, Mwaka 2000 aligombea na kushinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akashinda tena mwaka 2007 na kushinda na tangu wakati huo aliteuliwa kuingia kwenye Kamati Kuu ya CCM hadi hivi sasa.
Nguvu
Dk Mwinyi ni mmoja kati ya mawaziri wenye rekodi za kuwa shahada tatu za ubobezi wa taaluma na elimu ya juu katika fani moja. Amesoma kwa uhakika na ni mtu mwenye uwezo wa kutumia stadi za ubobezi wake kujenga weledi wa jumla unaomfanya atoe uongozi wa kudumu hadi hivi, nina hakika kuwa ubobezi wake utaendelea kumbeba hata kwenye uteuzi wa sasa.
Jambo la pili ni uzoefu wa kibunge wa miaka 15 unaoambatana na uzoefu wa uwaziri kwa miaka 15. Mwinyi ana rekodi nyingine tena, ni kati ya wabunge walioweza kukaa bungeni kwa vipindi vitatu mfululizo (2000 – 2015) na tena anaongeza kipindi cha nne (2015 -2020). Huyu ni mmoja kati ya viongozi wa zama za sasa waliokaa muda mrefu kwenye utumishi wa ngazi ya juu na ikumbukwe kwamba muda wote huo amekuwa kwenye nafasi za uwaziri. Uzoefu wake wa pamoja unamtofautisha na mawaziri wengine wengi wanaojifunza kazi na huwenda ukamjengea kujiamini zaidi na kufanya vizuri zaidi.
Tatu ni haiba, Dk Mwinyi ni mtu mwenye kupenda kuwa na watu wa chini, askari mmoja wa cheo cha chini amenijulisha kuwa kuna siku amekaa na Dk Mwinyi katika kikao cha rafiki wa familia na hadi kikao kinaelekea mwishoni na kufungwa ndipo akadokezwa yule ndiyo bosi wake (yaani waziri anayeongoza ulinzi). Askari yule anasema alishtuka sana kwa sababu hakuamini kama Mwinyi angekuwepo pale, mahali pa chini sana, lakini utulivu wake na “kutojifanya anajua kila kila kitu” vingemfanya mtu yeyote amuone Mwinyi kama mtu wa kawaida sana. Kama Mwinyi anaendeleza uongozi wa namna hii anaweza kuendelea kuwamudu askari na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama wa ngazi za juu na chini kwa mafanikio.
Udhaifu
Haiba mojawapo ya Mwinyi ni kuonekana kama mtu mpole sana na anayeweza kutafsiriwa kuwa hana maamuzi ya “purukushani na ufuatiliaji usiokwisha”, kwa staili aliyoanza nayo JPM na waziri mkuu wake, ya kufanya ziara za kushtukiza huku na kule, na kutoa maamuzi hapa na pale (mambo ambayo Mwinyi hayawezi) vinaweza kutafsiriwa kama waziri huyu haendani na haiwezi kasi ya utendaji ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Lakini ukweli unabakia kwamba kama mtu anao uwezo wa kufanya maamuzi na ameyasimamia kwa miaka 15 katika ngazi za juu za utendaji, hawezi kushindwa kufikia malengo makubwa kwa kuzingwa na haiba yake inayoweza kuchukuliwa kama “upole na kufanya mambo polepole sana”. Huwenda unapoongoza vyombo vya ulinzi na usalama haupaswi kuwa mtu wa pupa na maamuzi ya haraka yanayoweza kuathiri maisha ya watu, ndiyo maana pia sioni yale matarajio ya watu ya “ziara za kushtukiza, matamko ya kusimamisha watu kazi na pilikapilika nyingi” zikifanywa na waziri huyu “wanajeshi wako tayari muda wote na ukidhani kama unaweza kuwashtukiza, utashtukizwa wewe”.
Matarajio
Matarajio ya Dk Mwinyi ni makubwa, kuendeleza kazi yake aliyojiachia chini ya utawala wa JK akajipasia wakati wa utawala wa Magufuli. Ikumbukwe kwamba huyu ndiye mwanasiasa aliyeweka rekodi ya kurudishwa kuongoza wizara hii mara nyingi kuliko mwingine yeyote, ameondolewa hapa na kurudishwa mara tatu. Sina hakika kama ameweka rekodi ya kukaa muda mrefu kuliko wengine.
Kwa sababu wizara hii ni nyeti sana, watendaji nilioongea nao wanaamini kuwa mtu waliyeletewa ni sawasawa, wanasema wanamfahamu vizuri na kwamba wanajua yeye anajitambua na amejipanga kutoa uongozi unaoweza kupelekea mabadiliko wanayoyataka, ambayo yalikosekana katika awamu zilizopita. Kwa sababu Mwinyi si mgeni mahali hapa wengi wanatarajia kuwa ataanza utekelezaji wa mambo mbalimbali mara moja kwani hana jipya la kujifunza, hakabidhiwi ofisi upya.
Changamoto
Moja kati ya changamoto kubwa zinazoikabili wizara hii ni ulinzi wa mipaka ya nchi. Hivi karibuni sote tunajua kulikuwa na sakata la wahamiaji haramu kuondolewa nchini na kurejeshwa katika nchi zao. Hawa wameingia hapa Tanzania kwa njia za panya na wenye jukumu la kuzia michezo hiyo ni wizara hii ikishirikianana na baadhi ya taasisi za wizara ya mambo ya ndani. Masuala ya wakimbizi na mahusiano yao na wananchi wa nchi yetu, ulinzi wao na mikakati ya muda mrefu ya kiulinzi ikiwahusisha yanaangukia pia kwenye wizara hii. Changamoto ya ugaidi unaoanzia mipakani na namna gani Tanzania itaendelea kufanywa kuwa salama dhidi ya ugaidi ni mambo yanayomkabili Dk Mwinyi. Bahati nzuri aliyonayo kwenye wizara hii ni kwamba hana msaidizi, kwa hiyo yeye ndiye kila kitu na atakuwa na wakati mwema kufanya maamuzi na kusimamia utekelezaji wake yeye mwenyewe bila kumtuma mtu.
Changamoto ya pili inayoikabili wizara hii ni mindombinu ya ulinzi ikihusisha pia uchakavu wa vifaa vya ulinzi, nyumba na maeneo ya makambi ya majeshi yetu. Kwa wale waliowahi kuishi kwenye kambi za jeshi kama mimi wanatambua kuwa nyumba za askari zilizojengwa miaka hiyo hazina ukarabati, nyingi zinaporomoka na kupotea, zingine zimechoka sana, ni kama vile wizara haina bajeti ya kufanya marekebisho ya nyumba hizi. Askari wengi hivi sasa wako mitaani, askari wa vyeo vya chini na juu, ni hatari mno kwao na kwa familia zao kuendelea kuishi mitaani, dunia yote hii, dhana ya vyombo vya ulinzi ni watendaji wake kuishi katika sehemu zao maalum.
Lakini pia uchakavu wa vifaa vya kijeshi unatishia uhai na maisha ya wananchi, wengi wanakumbuka milipuko ya mabomu Mbagala na Gongolamboto ambayo (pamoja na kwamba wizara inaweza kuwa inajua chanzo na haikitangazi kwa sababu za kiusalama) lakini ukweli unabakia kuwa moja ya sababu za milipuko ile ni uchakavu wa vifaa vyenyewe. Majeshi yetu yanahitaji vifaa vya kisasa na bora kuliko wakati mwingine wowote, kwa ujumla, miundombinu katika majeshi yetu ni kipaumbele kisichokwepeka.
Kuna changamoto ya muda mrefu ya migogoro kati ya vyombo vya ulinzi na wananchi. Migogoro hii ina pande mbili, kuna ule upande wa askari kufanyiwa maudhi na wananchi na kujichukulia sheria mikononi (kuwavamia na kuwapiga) na kuna ule upande ambapo vyombo vya ulinzi wa mipaka ya nchi vinahusishwa katika oparesheni za ndani ya nchi ambazo zingepaswa kufanywa na wizara ya mambo ya ndani.
Mfano mzuri katika jambo hili ni “sakata la gesi Mtwara” ambapo zilipotokea vurugu kati ya wananchi na polisi na ikaonekana polisi wanazidiwa, mamlaka za juu zikaagiza askari jeshi waingie mtaani. Kilichotokea huko sote tunajua, ilikuwa ni raia kupigwa na kuteswa, na hata Mkurugenzi wa kitaifa wa chama cha siasa alikamatwa bila sababu na kushikiliwa katika kambi ya jeshi huko mkoani Mtwara na kuteswa hadi kupoteza fahamu. Kama mamlaka za nchi zingelikuwa zinafuata utaratibu, polisi wanapozidiwa nguvu na raia mahali popote inaongezwa nguvu ya polisi, wao hujua muda gani watumie nguvu kiasi gani, askari jeshi wamefundishwa mafunzo tofauti sana. Mambo yote mawili niliyoyataja yanabakia kuwa kuhitaji utatuzi wa muda mrefu wa utulivu ili uhusiano mzuri ulipo kati ya raia na vyombo vya ulinzi hususani Jeshi na JKT uendelee.
Na mwisho, Dk Mwinyi na wizara yake wana kazi kubwa ya kuhuisha utendaji na mipango ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), jeshi hili lilianzishwa kwa sababu maalum na jina lake linasadifu kazi yake, kwa bahati mbaya hivi karibuni matakwa sahihi ya JKT yamekuwa yakizorota, inafikia wakati Serikali inatangaza kuwa haina bajeti ya kutosha kutoa mafunzo kwa vijana wote wenye sifa za kujiunga na JKT. Mafunzo yenyewe yamefanywa kuwa mafupi mno na kijana anapotoka huko anakuwa hajabobea vya kutosha kwenye masuala ya stadi za kazi.
Ifikie wakati muda wa JKT uongezwe na ukiachilia mbali kufundishwa masuala ya ulinzi na usalama, robo tatu ya muda unaobakia ihakikishwe kila kijana anayetoka huko walau amebobea kwenye eneo mojawapo la ufundi, kwamba akitoka huko akabidhiwe mathalani vifaa vya ujenzi wa nyumba na ajenge nyumba kama fundi. Tukifanya hivyo JKT itakuwa si tu sehemu ya kuimarisha ukakamavu kwa vijana, bali itakuwa ni Chuo bora cha Ufundi hapa Tanzania ambacho kitawapatia vijana ujuzi na uhakika wa ajira mara wanapohitimu.
Hitimisho
Uteuzi wa Dk Mwinyi kuendelea kuwa waziri kwenye baraza la JPM ulitegemewa na watu wengi na sikusikia ukipingwa kokote. Huyu anabakia kuwa mmoja wa wanasiasa muhimu sana wenye ushawishi katika siasa za muungano na ndani ya CCM lakini akiwa mkimya sana na mtulivu. Bado naamini kwamba siku CCM wakiamua kuwa mgombea wao wa urais atoke visiwani Zanzibar, huwenda Dk Mwinyi ndiye mwenye nafasi hiyo. Kwa hatua ya sasa namtakia kila la heri katika uongozi wa wizara aliyoizoea sana.

Kuhusu mchambuzi
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Adv Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri (M.A) ya Usimamizi wa Umma na Shahada ya sheria (L LB); +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com, https://www.facebook.com/JuliusSundayMtatiro/, - Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni