Wakala
wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kwa kushirikiana na Jeshi la
Polisi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Usalama wa Taifa wamekamata
madini yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 11.2 ambayo yalikuwa
yakitoroshwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA).
Hayo
yalisemwa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na
Mawasiliano wa TMAA, Mhandisi Yisambi Shiwa ambapo alieleza kuwa raia
mmoja wa kigeni na mwingine wa Tanzania walikamatwa wakiwa na madini
hayo bila kuwa na kibali chochote cha usafirishaji kama ambavyo Sheria
ya Madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza.
“ Raia
huyu wa kigeni ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi
kwani tayari ameshafunguliwa kesi mahakamani, alikuwa anasafiri kwenda
mji wa Bangkok Thailand na alikamatwa akiwa na madini ya aina mbalimbali
ikiwemo almasi, aquamarine, sapphire, green tourmaline, quartz na
rhodolite,” alisema Mhandisi Shiwa.
Aidha,
Mhandisi Shiwa alisema kuwa katika tukio la pili mtuhumiwa mwingine
raia wa Tanzania ambaye alikuwa anasafiri kwenda Ujerumani alikamatwa
akiwa na madini mbalimbali ikiwemo amethyst, moonstone cabochon,
rulilated quartz (cabochon), rulilated quartz(faceted), chrysoprase,
green tourmaline, rubi, red garnet, green quartz, zircon na rhodolite na
kufikishwa katika vyombo vya Dola.
Alisema
kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai mwaka 2015 hadi Januari 13
mwaka huu kumekuwepo na jumla ya matukio 14 ya utoroshaji madini ambapo
madini yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.4 (zaidi ya Shilingi
Bilioni 3.2) yalikamatwa na wakaguzi wa Wakala kupitia Madawati ya
Ukaguzi yaliyopo katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam (JNIA),
Kilimanjaro (KIA) na Mwanza ambapo yote yalitaifishwa na Serikali.
Mhandisi
Shiwa ametoa rai kwa Umma kujiepusha na shughuli za utoroshaji na
biashara haramu ya madini kwani hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa
yeyote atakayebainika au kukamatwa akijihusisha na shughuli hizo ikiwemo
kutaifisha madini yaliyokamatwa.
Vilevile
Mhandisi Shiwa alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini inatoa motisha kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa kwa Kamishna wa
Madini ama Wakala za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya madini
ambazo zitawezesha ukamataji wa madini, atazawadiwa fedha taslimu ambazo
ni asilimia 5 ya thamani ya madini yatakayokamatwa na kunadiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni