Dodoma. Mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika jana ulizua kizaazaa na kumlazimisha Spika Anne
Makinda kuahirisha kikao baada ya kukosekana utulivu ndani ya Ukumbi wa
Bunge.
Kikao hicho kiliahirishwa muda mfupi baada ya
kipindi cha maswali na majibu wakati Bunge lilipotakiwa kukaa kama
kamati kumalizia kiporo cha Muswada wa Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa
za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015 ambao mchakato wa kuupitisha
haukukamilika juzi kutokana na muda kuisha.
Ilikuwa ni kama marudio ya hali ilivyokuwa
mwishoni mwa mwaka jana wakati wabunge wa upinzani waliposimama na
kuweka mazingira ambayo yalizuia shughuli za chombo hicho kuendelea
wakati wa kujadili sakata la escrow.
Jana, sakata hilo lilitokea baada ya Spika Makinda
kuweka sharti la kutoa mwongozo ulioombwa na Mnyika aliyetaka kujua
sababu za uongozi kuwasilisha miswada mitatu kwenye shughuli za jana
licha ya wabunge wa pande zote mbili kuipinga kwa kuwa haina haraka.
Kutokana na majibu hayo, wabunge wa upinzani
walisimama na kuanza kupiga kelele wakipinga kitendo hicho cha uongozi
wa Bunge huku wakisema; “muda wa kuburuzana umekwisha.”
Hata Spika Makinda alipojaribu kuwatuliza walipiga
kelele na kumfanya kiongozi huyo wa chombo cha kutunga sheria kutangaza
kuahirisha shughuli za Bunge.
Hali ilivyokuwa
Mwongozo wa Mnyika ulitokana na ratiba ya shughuli Bunge kuonyesha kuwa kulikuwa na miswada minne iliyotakiwa kujadiliwa.
Hiyo ilikuwa ni Muswada wa Sheria ya Kuwalinda
Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015 ambao ulifikia ngazi
ya Bunge kukaa kama kamati kuupitisha, Muswada wa Sheria ya Petroli wa
mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi
na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Uchimbaji.
“Mheshimiwa Spika, naomba mwongozo wako kwa
kutumia kanuni ya 53 (1) na (6) ambazo zinasomwa pamoja na kanuni ya 86
katika vifungu vya 1,5,6, kwamba Bunge lako limekiuka kanuni kwa kuleta
hoja juu ya hoja,” alisema Mnyika.
Alipopewa nafasi ya kufafanua hoja yake, Mnyika
alisema: “Tarehe 29 Bunge lako lilipokea semina juu ya miswada hii
mitatu ambayo leo imeingizwa tena bungeni na wabunge kwa kauli moja,
bila ya kujali itikadi za vyama, tulipinga jambo hili lakini leo tunaona
mmeleta tunaomba ufafanuzi,”
Alisema na kumtaka Spika atoe ufafanuzi hapohapo kwa kuwa jambo hilo lilikuwa ni muhimu.
Majibu ya Spika
Spika Makinda alisimama na kumtaka kwanza Mnyika
kuondoa maneno ya amri kwani vinginevyo asingeweza kutoa jibu lolote kwa
madai kuwa hawezi kuamrishwa.
“Ondoa maneno ya kuamrisha hapa, nasema ondoa
maana nyinyi tabu yenu ni kuwa hamjajiandaa kwa shughuli hii, tena
ikumbukwe kuwa tulikaa kikao cha Kamati ya Uongozi mara baada ya semina
ile na Mheshimiwa (David) Silinde alikuwapo, sasa mnasemaje tena?”
alisema Makinda.
Hata hivyo, kauli yake ni kama iliongeza hasira
kwa wabunge wa upinzani ambao walisimama na kuanza kupiga kelele
wakisema lazima miswada hiyo iondolewe.
Kuona hivyo, Makinda alisimama na kusema: “Sasa amueni ninyi maana mliomba mwongozo au amueni wenyewe sasa.”
Kelele za wabunge zilizidi kiasi cha kuibuka
majibizano kutoka kwa wabunge wa pande zote na wakati huo tayari Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Jenister Mhagama akiwa
amesimama huku wapinzani wakiimba “tumechoka kuburuzwa, mnataka mafisadi
kututawala.”
Ndipo Spika akasema: “Waheshimiwa wabunge, ninaahirisha shughuli za Bunge hadi baadaye.”
Alipomaliza kuahirisha, wabunge wa upinzani
walibaki ndani na kufanya kikao cha dakika chache, huku wabunge wa CCM
wakitoka na moja kwa moja kwenda kukutana kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa.
Lissu azungumzia sakata
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa upinzani,
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliwaambia waandishi
wa habari kuwa miswada hiyo ni migumu na kuipitisha kwa haraka wakati
nchi haiko kwenye machafuko, haitawezekana.
“Muswada mmoja una vifungu zaidi ya 300 wakati
vipengele vya kurekebisha ni zaidi ya 1,000, hata mimi mwanasheria
ninahitaji miezi zaidi ya mitatu kumaliza kazi hiyo. Sasa, haraka hii ni
ya nini?” alihoji Lissu.
Lissu alisema kwa vyovyote vile hawatakubali kwani
wamebaini kuwa kuna shinikizo ndani ya Serikali kulazimisha kuipitisha
miswada hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni