Hakimu Mwakalinga siku alipohukumiwa
kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Rungwe. Leo amehukumiwa tena kunyongwa mpaka kufa katika mauaji ya
mlemavu wa ngozi Henry Mwakajila.
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mbeya leo hii
imewahukumu kunyongwa mpaka kufa watu wanne kati ya watano waliomuua
Henry Mwakajila (17) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino).
Waliohukumiwa kunyongwa mpaka kufa ni
Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga na Gerard Korosso
Kalonge (wakazi wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje), na Leonard
Msalage Mwakisole na Hakimu Mselem Mwakalinga (wakazi wa Kiwira wilayani
Rungwe).
Mshtakiwa wa nne, Mawazo Philemon
Figomole, ameachiliwa huru na mahakama hiyo baada ya ushahidi wa upande
wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasi na shaka kwamba alihusika katika
mauaji hayo.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo ya mauaji
yenye kumbukumbu Namb. KIW/IR/49/2008 na PI 5/2013, Jaji wa Mahakama Kuu
Dk. Revila, amesema mahakama imejiridhisha pasi na shaka na ushahidi wa
upande wa mashtaka kwamba washtakiwa hao wanne walitenda kosa hilo na
hivyo wanastahili adhabu hiyo.
Hii ni kesi ya saba ya mauaji ya albino
kutolewa hukumu ambapo mpaka sasa jumla ya watuhumiwa 15 wamehukumiwa
kunyongwa mpaka kufa. Ililezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo Februari 5,
2008 majira ya saa 12:00 na saa 1:00 jioni huko katika Kijiji cha
Ilolo, Kata ya Kiwira, tarafa ya Ukukwe, wilayani Rungwe katika Mkoa wa
Mbeya, washtakiwa hao walimteka nyara kijana Henry Mwakajila, ambaye ni
mlemavu wa ngozi aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika Shule ya
Sekondari Ukukwe na kisha kumuua.
Wakati wa mwenendo wa kesi, ilielezwa na
mashahidi wa upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa wa kwanza Asangalwisye
Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga ambaye ni mganga wa jadi, mkazi
wa Kijiji cha Mbembati, Wilaya ya Ileje, alikutwa na utumbo unaodhaniwa
kuwa wa binadamu na ulipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali
ukathibitika kwamba ni utumbo wa marehemu Henry.(VICTOR)
Mshtakiwa wa pili, Gerard Korosso Kalonge
wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje alikutwa na vidole vinne na
mifupa kumi (10) vyote vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu na baada ya
uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali ilibainika kwamba ni viungo vya
marehemu Henry Mwakajila.
Ilielezwa pia kwamba, washtakiwa Leonard
Msalage Mwakisole, Mawazo Philemon Figomole na Hakimu Mselem Mwakalinga
ndio waliodaiwa kumteka nyara mtoto huyo na kumuua, kisha kupeleka
viungo kwa mganga wa kienyeji Asangalwisye Kayuni.
Mshtakiwa wa tano, Hakimu Mselem
Mwakalinga, tayari alikwishahukumiwa kunyongwa katika kesi nyingine ya
mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja,
ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake. Hukumu ya kesi hiyo
namba 131/2012 ilitolewa Novemba 13, 2013 ambapo inaelezwa kwamba
watuhumiwa walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika kijiji cha
Mpandapanda, Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Ingawa watuhumiwa walikuwa wanne, lakini
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua iliwahukumu
kunyongwa mpaka kufa mshtakiwa wa kwanza Hakimu Mwakalinga na mshtakiwa
wa pili Daudi Mwasipasa kwa maelezo kwamba walihusika moja kwa moja na
mauaji hayo ya kukusudia.
Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili
yeye alitiwa hatiani kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja
baada ya kutoka kufanya mauaji wakati mshtakiwa namba nne Kelvin
Myovela alitiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika katika
mauaji hayo ingawa hakusika na kitendo hicho moja kwa moja, hivyo wote
wawili walihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, Myovela tayari alikwishahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na silaha kinyume cha sheria.
Inadaiwa kwamba, chanzo cha mauaji hayo
ya John Mwankenja, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
Wilaya ya Rungwe, kilitokana na kiongozi huyo kufahamu kwamba hao ndio
waliomuua mlemavu wa ngozi Henry Mwakajila, hivyo aliuawa ili kupoteza
ushahidi.CHANZO:www.brotherdanny.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni