TANGAZO

TANGAZO

Jumatano, 1 Julai 2015

MAJINA YA WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA TANO 2015 YATANGAZWA

Jumla ya wanafunzi 18,751 kati ya 73,754 (asilimia 74.58) waliofanya mitihani ya kidato cha nne mwaka jana wamekosa nafasi za masomo za kujiunga kidato cha tano na vyuo vya ufundi mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali.
Miongoni wa sababu hizo ni ufinyu wa nafasi za shule, kushindwa kupata ufaulu wa masomo waliyochagua, umri mkubwa wa watahiniwa wa kujitegemea pamoja na kukosa sifa za kuchaguliwa, huku muhula wa kwanza wa kujiunga kidato cha tano ukitarajiwa kuanza Julai 18, mwaka huu.
Aidha, wanafunzi 479 wakiwamo wavulana 332 na wasichana 147 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi mwaka huu, huku idadi ya wanafunzi hao ikiongezeka kutoka 472 mwaka 2014 hadi 479 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa, alisema ufaulu umeongezeka na kwamba idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi imeongezeka kutoka wanafunzi 117 mwaka 2014 hadi 147 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 25.64.
Alisema kati ya wanafunzi ambao hawakuchaguliwa, wavulana ni 13,216 na wasichana ni 3,219.
Hata hivyo, alisema wanafunzi hao watadahiliwa na Baraza la Taifa la Ufundi (Nacte) kwenye fani mbalimbali zikiwamo za ualimu, afya, maendeleo ya jamii na kilimo.
Majaliwa alisema kati wanafunzi 55,003 waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano na mafunzo ya ufundi mwaka huu, wavulana ni 31,700 na wasishana ni 23,303 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 918 ikilinganishwa na wanafunzi 54,085 waliochaguliwa mwaka jana.
Alisema wanafunzi hao wamechaguliwa kujiunga kidato cha tano katika shule 277 zikiwamo 29 zilizopangiwa wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Alisema wanafunzi 29,744 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya sayansi na hisabati wakiwamo wavulana 18,294  na wasichana 11,450 sawa na asilimia 54.08.
Pia, alisema wanafunzi 25,259 wakiwamo wavulana 13,406 na wasichana 11,853(45.92) wamechaguliwa kujiunga na masomo ya sanaa na biashara.
Naibu Waziri huyo alisema ufaulu wa watahiniwa wa mwaka 2014 kwa kuzingatia madaraja yaani GPA ya 5.0 hadi 1.6 ni watahiniwa 73,754 sawa na asilimia 37.48 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo mwaka jana.
Alisema kuna ongezeko la ufaulu wa asilimia 17.17 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2013 ambayo watahiniwa walifaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu, huku idadi ikiwa 71,527 sawa na asilimia 20.28 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo.
Majaliwa alisema muhula wa kwanza kwa masomo ya kidato cha tano mwaka huu utaanza Julai 18 na kwamba wanafunzi wote wamepangwa katika shule zenye miundombinu na walimu wa masomo husika.
Aliwataka wanafunzi waliochaguliwa kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati na kuonya watakaoshindwa kuripoti shuleni zaidi ya siku 14 nafasi zao zitachukuliwa na wanafunzi ambao wamekosa nafasi.
Alieleza kuwa, uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga kidato cha tano na vyuo vya ufundi umefanyika kwa kutumia mfumo wa kompyuta na kwa kuzingatia machaguo ya wanafunzi, ufaulu wa nafasi zilizopo katika shule husika na kusistiza hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule.
Mwaka juzi wanafunzi 54,085 (asilimia 75.61) kati ya 404,083 (asilimia 94.48) waliofanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne Tanzania Bara walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za sekondari za serikali na vyuo vya ufundi, huku 16,800 wenye sifa zinazotakiwa wakikosa kuchaguliwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo ufinyu wa nafasi.
: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni