TANGAZO

TANGAZO

Jumatano, 11 Novemba 2015

SAMATTA AMUAHIDI KITU KIZURI RAIS MAGUFULI MGENI RASMI STARS V ALGERIA JUMAMOSI TAIFA



picha na Bin Zuber
WAKATI imetangazwa rasmi, Rais wa Jamhuri ya Dk John Pombe Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na Algeria, mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Mbwana Samatta amesema amepania makubwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake mchana wa leo mjini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa, Saidy Mecky Sadick amesema kwamba Rais Magufuli ndiye mgeni rasmi katika mchezo huo.
Mecky Sadick amesema Rais huyo mpya wa awamu ya tano amekubali wito huo ili kujitokeza kuongoza kampeni ya kuwahasisha wachezaji wa Tanzania kuifunga Algeria Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi.


Mbwana Samatta amempa ahadi nzuri Rais Dk John Pombe Magufuli kuelekea mchezo wa Taifa Stars na Algeria Jumamosi   

Aidha, Samatta kwa upande wake amesema kwamba
baada ya kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na klabu yake, TP Mazembe mjini Lubumbashi, DRC sasa nguvu zake anazielekeza Taifa Stars.
“Nataka kuisaidia timu yangu ishinde Jumamosi na pia ishinde mchezo wa marudiano ili tusonge mbele kwenye mbio hizi,”amesema Samatta.
Taifa Stars itamenyana na Algeria, ‘Mbweha wa Jangwani’ Jumamosi kabla ya kurudiana Novemba 17 mjini Algiers na mshindi wa jumla ataingia kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2018 Urusi.
Samatta ataingia katika mchezo huo akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe, klabu ambayo anacheza pamoja na Mtanzania mwenzake, ThomaS Ulimwengu ambaye yupo pia timu ya taifa.
Mchezo huo uliofanyika Jumapili Uwanja wa Mazembe Lubumbashi, wenyeji walishinda 2-0 dhidi ya USM Alger mabao ya Samatta na Rogger Asalle raia wa Ivory Coast na kufanya ushindi wa jumla wa 4-1, baada ya awali TP kushinda 2-1 Algiers.
Na Samatta pia ameibuka mfungaji bora wa michuano hiyo msimu huu baada ya kufunga mabao saba sawa na Bakri Al-Madina wa El-Merreikh ya Sudan.
Hii maana yake huu unakuwa mwaka wa pili mfululizo, Tanzania inatoa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa, baada ya mwaka jana Mrisho Khalfan Ngassa kuongoza pia akiwa na klabu ya Yanga SC, kabla ya kuhamia Free State Stars ya Afrika Kusini msimu huu.
Ngassa alifunga mabao sita sawa na El Hedi Belameiri wa Setif, Haythem Jouini wa Esperance na Ndombe Mubele aliyekuwa AS Vita ya DRC, sasa Al Ahly, ingawa Yanga SC iliishia hatua ya 32 Bora.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni