Elius Maguri, amejikuta akichezea mkeka ndani ya kikosi cha Stand United licha ya kuwa kwenye kiwango bora kwa sasa
Mshambuliaji
wa Stand United Elius Maguli siku za hivi karibuni amekuwa haonekani
dimbani kutokana na kuchezea mkeka ndani ya kikosi cha Stand United
chini ya kocha mfaransa Patrick Liewig.
Baada ya kuligundua hilo, mtandao huu uliamua kumtafuta mwenyekiti wa
klabu hiyo Amani Vicent kumuuliza kama striker huyo ambaye alianza ligi
kwa kasi huku akitupia kambani mfululizo anatatizo lolote
linalosababisha asugue bechi.
“Elius Maguli hana tatizo na uongozi wa Stand Unitd na kutokupangwa
kwake kunatokana na program ya mwalimu mwenyewe alivyojiwekea maana yeye
ndiyo mkuu wa benchi la ufundi, ikumbukwe Maguli aliondoka kwenda
kufanya majaribio huko Misri aliporudi alikuwa amechelewa kujiunga na
timu na vilevile mwalimu anasema yeye hakuwa ameagwa”, amesema
mwenyekiti wa Stand United.
“Lakini siyo kesi sana, kwasababu program za kupanga kikosi zinakuwa
chini ya mwalimu, kwahiyo sababu inawezekana ikawa hiyo lakini mechi ya
Mtibwa alicheza, mechi ya FA Cup na Mwadui aliingia akacheza kwahiyo
nadhani lipo kwenye mikono ya kocha kama alikuwa amekwazwa na hilo au
la, lakini sisi kama uongozi tulikubali akafanye trial maana kule kwenye
klabu ya Zamalekh kama angekuwa amefaulu basi ilikuwa ni moja ya
maendeleo kwake na klabu ya Stand kwasababu wachezaji kama hawa
wanacheza kwa ajili ya kutafuta maisha lakini pia kulisaidia taifa”.
“Kwahiyo nafikiri kulikuwa na mawasiliano madogo kati ya kocha na
uongozi nafikiri hilo pia limekuwa sababu lakini sababu nyingine ni za
kocha mwenyewe kwasababu anakikosi kipana anaweza kufanya anavyoweza
yeye kama mkuu wa benchi la ufundi”.
Maguli alikuwa kwenye kiwango bora tangu alipojiunga na Stand United
baada ya kupigwa chini na ‘wekundu wa Msimbazi’ Simba. Maguli aliongoza
orodha ya wafungaji kwenye ligi ya VPL na kupelekea kuitwa kwenye
kikosi cha Taifa Stars lakini siku za hivi karibuni amejikuta akichoma
mahindi kwenye benchi licha ya kuwa na kiwango cha hatari lakini
inaonekana hakuna maelewano kati ya Maguli na kocha wa timu hiyo Patrick
Liewig
Chanzo:Shafii Dauda
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni