CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinatarajiwa kuzindua kampeni zake za urais,
ubunge na udiwani nchi nzima katika viwanja vya Jangwani leo, katika
mkutano utakaorushwa moja kwa moja na televisheni na redio mbalimbali
nchi nzima.
Katika uzinduzi huo, CCM pia inatarajiwa kuweka ilani yake ya uchaguzi
hadharani, itakayonadiwa na mgombea urais wake, Dk John Magufuli na
wagombea wengine wa ubunge na udiwani nchi nzima.
Moja ya mambo ambayo CCM inatarajiwa kufafanua ni matumaini makubwa ya
uwezo wa mgombea wake katika kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo,
kutokana na historia yake ya utendaji ndani ya Serikali katika nafasi
mbalimbali alizokabidhiwa, ikiwemo Waziri wa Ujenzi.
Wageni mbalimbali pia wamealikwa kuhudhuria uzinduzi huo vikiwemo pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa CCM Mkoa, Juma Simba
alisema vile vile wanatarajia wageni kutoka ndani na nje ya jiji la Dar
es Salaam kuhudhuria mkutano huo leo.
“Tumetuma mialiko ya mkutano wa kesho (leo) sio tu kwa wana CCM wenzetu
bali pia kwa vyama vingine vya siasa ikiwa ni pamoja na kwa vyama vya
‘Ukawa’,” alisema.
Simba alisema mkutano huo utakuwa mkubwa na wa aina yake ambapo viongozi
mbalimbali wa chama wanatarajiwa kushiriki na kwamba mkutano huo ratiba
yake itaanza asubuhi saa tatu kwa burudani kutoka kwa wasanii
mbalimbali na wananchi kuendelea kuwasili uwanjani.
Sifa za Magufuli Mgombea huyo amekuwa akitajwa kuwa na sifa ya
mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, ambapo Mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete alimpachika jina “Tingatinga”.
Rais Kikwete alimpachika Magufuli jina hilo, baada ya kutangazwa
kuwashinda makada wengine wawili waliokuwa wakiwania kuteuliwa kuwania
urais kupitia chama hicho katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika
Dodoma.
“Kila mtu anaitwa jembe lakini huyu ni zaidi ya jembe. Ni tingatinga…
Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumilii ujinga, ni mtu ambaye anataka
kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza,” alikaririwa akisema.
Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake
akisema kuwa alipokuwa akifuatilia makandarasi kwenye miradi ya ujenzi,
alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na
makubaliano.
Baadhi ya watu waliofanya naye kazi wamekaririwa wakisema iwapo
atachaguliwa kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri
huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni