Kigoma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameanza ziara mkoani Kigoma huku akiahidi
kuanza ujenzi wa reli mpya ya kisasa ya viwango vya ‘standard gauge’,
itakayosaidia kuimarisha biashara ya kusafirisha mizigo kutoka Dar es
Salaam kwenda nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC),
kupitia Bandari ya Kigoma.
Tamko
la Waziri Mkuu Majaliwa inaashiria kuanza kwa utekelezaji wa vipaumbele
25, ikiwamo ujenzi wa reli ya kati, alivyovitoa Rais John Magufuli
(wakati huo akiwa mgombea urais wa CCM), Agosti 24, wakati wa uzinduzi
wa kampeni zake kwenye Viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na wakazi wa Kigoma katika Mwalo wa Kibirizi, Waziri Mkuu Majaliwa
alisema mradi huo utaambatana na ujenzi wa bandari kavu eneo la Katosho
mjini Kigoma, kwa ajili ya kushusha mizigo inayosubiri kwenda nje ya
nchi.
“Lazima
tujenge reli ya kisasa na tumezindua ujenzi wa reli ya urefu wa
kilomita mbili. Huwezi kuimarisha bandari kama reli itakuwa imechoka na
hii ilijengwa miaka 100 iliyopita, sasa imezeeka haifai, ndiyo maana
tumeamua kutumia fedha nyingi kuhakikisha mradi huu wa reli ya kisasa na
ujenzi wa bandari unakamilika kwa wakati,” alisema Waziri Mkuu
Majaliwa.
Katika
maelezo yake hayo Majaliwa alipokea kilio cha wakazi wa Katosho
inakotakiwa kujengwa bandari kavu wanaolalamika kupunjwa malipo ya fidia
ya nyumba na mazao, aliwahakikishia kuwa mchakato wa kutathmini
unarudiwa hivyo aliwashauri wananchi waliopokea fedha za fidia kuhama
ili kupisha ujenzi wa bandari.
Waziri
Mkuu Majaliwa aliwataka wavuvi na wafanyabiashara kutumia fursa ya
Mwalo wa Kibirizi, ambalo linapokea mazao ya uvuvi na kuyachakata kwa
ajili ya kuingia sokoni, jambo litakalosaidia kuinua uchumi na kuongeza
thamani ya mazao hayo.
Alisema
Serikali itatafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuuza
samaki na dagaa wanaovuliwa kutoka Ziwa Tanganyika na kuwezesha wavuvi
kujiongezea kipato, hali itakayowafanya wawe na uwezo wa kununua zana
bora za uvuvi na kuongeza kiwango cha uvuvi.
Pia
aliahidi kumuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa
Polisi (IGP), Ernest Mangu kuongeza ulinzi Ziwa Tanganyika ili
kupambana na maharamia wanaopora zana za uvuvi, ambapo pia amemuagiza
mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya kufanya kikao na Balozi wa Congo
DRC ili kuona njia bora ya kushirikiana kupambana na maharamia.
CHANZO:MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni