Mwanza.
Ugonjwa wa kipindupindu umeendelea kuzitesa Wilaya za Nyamagana na Magu
mkoani hapa, baada ya idadi ya wagonjwa kuongezeka na kufikia 17, huku
mtu mmoja akipoteza maisha wilayani Magu.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa, Dk Rwekyendela Onesmo
alisema licha ya jitihada zinazofanywa, ugonjwa huo unazidi kuzikumba
baadhi ya wilaya za mkoa huo.
“Kwa
sasa tunao jumla ya wagonjwa 17 kati yao Nyamagana na Magu wapo wanane
kwa kila wilaya na Ilemela yupo mgonjwa mmoja kwa sasa,” alisema.
Dk
Onesmo alisema, hali hiyo inaufanya mkoa huo kuwa na watu waliougua
kipindupindu kufikia 926, huku vifo vikiwa 25 tangu uliporitiwa kwa mara
ya kwanza katika Wilaya ya Ukerewe, Septemba mwaka huu.
Alisema kwamba jana mtu mmoja alipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo wilayani Magu.
Mganga
huyo alisema kutokana na idadi ya wagonjwa kuongezeka imewalazimu
kuandaa kituo kingine cha kuhudumia wagonjwa katika Wilaya ya Nyamagana.
“Awali,
tulikuwa na kituo kimoja cha Igoma, ila kutokana na hali inavyoendelea
imetupasa kuwa na kituo kingine katika Kituo cha Afya cha Mkolani baada
ya kuona wagonjwa wengi wanatokea maeneo ya Buhongwa ili tuondoe
usumbufu wa kuwasafirisha,” alisema Dk Onesmo.
Wakati
ugonjwa huo ukiendelea kushika kasi, Jiji la Mwanza limeanza kuzuia
uuzwaji wa vyakula vinavyotembezwa mitaani na magengeni, maji ya viroba,
matunda yaliyomenywa na pombe za kienyeji.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Adam Mgoye alisema atakayekaidi agizo hilo watachukua hatua za kisheria.
Hatua
hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliyepinga marufuku uuzaji wa
matunda holela ili kutokomeza kipindupindu.
Akizungumza
hivi karibuni, Mwalimu aliagiza waganga wakuu na wakurugenzi wa
halmashauri za wilaya kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara wanaouza
vyakula bila kuzingatia usalama wa walaji.
Aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha matunda hayauzwi sehemu za wazi na maeneo yanayohatarisha usalama wa afya za watu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni