Waliokuwa wagombea ubunge, Jimbo la Vwawa, Fanuel Mkisi (wa pili kutoka kulia) na John Mwambigija (wa pili kushoto) wa jimbo la Rungwe, wote wa Chadema, wakiwa ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya jana wakisubiri kusikiliza kesi zao walizofungua za kupinga matokeo yaliyowapa ushindi wagombea wa CCM katika majimbo hayo.
Mbeya. Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, imetupilia mbali shauri la kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi wa ubunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe(CCM).
Kesi
ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa jimbo hilo ilifunguliwa na
aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chadema, Abraham Mwanyamaki baada ya
kushindwa kulipa Sh3 milioni ambazo ni dhamana ya kesi kwa
anaowalalamikia.
Sheria
ya kesi za kupinga matokeo ya ubunge inamtaka mlalamikaji kulipa
dhamana ya Sh5 milioni kwa kila anayemlalamikia, ambapo Mwanyamaki
alitakiwa kulipa jumla ya Sh15 milioni kwakuwa aliokuwa akiwalalamikia
walikuwa watatu.
Hata
hivyo Mwanyamaki baada ya kuomba huruma ya mahakama alipunguziwa hadi
Sh1 milioni kwa kila mlalamikiwa. Jumla alitakiwa alipe Sh3 milioni.
Pia
Mahakama hiyo imeamuru Mwanyamaki kulipa fidia ya gharama za
walizotumia walalamikiwa katika kesi hiyo, ambao ni Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Kyela, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Dk Mwakyembe.
Mwanyamaki
ni miongoni mwa waliyokuwa wagombea wa mkoani Mbeya, ambao walifungua
kesi mahakamini hapo, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Wengine
ni Liberatus Mwang’ombe (Chadema) dhidi ya mbunge Haroon Pilmohamde wa
CCM (Mbarali), John Mwambigija (Chadema), dhidi ya Saul Amoni wa CCM
(Rungwe), Dk Luca Siame (CCM) dhidi ya David Silinde wa Chadema (Momba),
Adam Zella (Chadema) dhidi ya Oran Njeza wa CCM (Mbeya Vijijini) na
Fanuel Mkisi (Chadema) dhidi ya Jophet Hasunga wa CCM (Vwawa).
Jaji
wa mahakama hiyo, Atuganile Ngwala alitoa uamuzi huo jana mahakamani
hapo baada ya wakili wa Mwanyamaki, Benjamini Mwakagamba akisaidiana na
Adrian Mhina kudai mahakamani hapo kwamba mteja wao alishindwa kutoa
kiasi hicho alichotakiwa kulipa ili kesi ya msingi iweze kuendelea,
hivyo wanaiachia mahakama iweze kutoa uamuzi wake juu ya suala hilo.
Baada
ya maelezo Jaji Ngwala akatoa nafasi kwa wakili aliyekuwa akimtetea Dk
Mwakyembe, Mpale Mpoki aliiomba mahakama imuamuru Mwanyamaki awalipe
gharama walizotumia tangu kesi ndogo ianze kulizikilizwa mahakamani
hapo.
Akitoa
uamuzi huo, Jaji Ngwala alisema ameridhika na hoja ya wakili Mpoki, na
kusema licha ya Mwanyamaki kushindwa kulipa gharama hiyo na kesi kufutwa
haina maana kwamba hatatakiwa kulipa gharama nyingine.
“Mahakama
inamtaka mdai (Mwanyamaki) kulipa gharama zote kwa washtakiwa wote
watatu aliowashtaki kwani ndiye aliyeleta pingamizi hilo. Na kushindwa
kwake kulipa kiasi cha Sh3 milioni tatu na kesi kuondolewa mahakamani
hapa haimaanishi hatatakiwa kulipa fidia hizo,” alisema Jaji Ngwala.
Katika
hatua nyingine, Jaji Ngwala alisema walalamikaji wengine walikamilisha
taratibu zote walizotakiwa ikiwamo kulipa Sh3 milioni, ili kesi ya
msingi ianze kusikilizwa kama ambavyo walioomba kwenye kesi ndogo ya
kuomba kupunguziwa gharama kutoka Sh5 milioni kwa kila mshtakiwa hadi
Sh1 milioni kwa kila mmoja.
Alisema
Januari 7 kesi hizo zitapangiwa majaji kwa ajili ya kuanza kusikilizwa,
ambapo walalamikaji, Liberatus Mwang’ombe wa Jimbo la Mbarali, John
Mwambigija wa Rungwe, wanatetewa na mawakili Benjamini Mwakagamba na
Adrian Mhina, Fanuel Mkisi wa jimbo la Vwawa anatetewa na mawakili
Magreth Lyatuu na Boniface Mwabukusi.
CHANZO :MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni