TANGAZO

TANGAZO

Jumanne, 29 Desemba 2015

Wanafunzi 70 wapoteza mwelekeo wa shule baada ya bomoabomoa Dar


PICHA:MWANANCHI

Dar es Salaam. Zaidi ya wanafunzi 70 wa shule za msingi na sekondari huenda wakashindwa kuendelea na masomo, baada ya familia zao kukumbwa na bomoabomoa kwenye Bonde la Mto Msimbazi, na kukosa mahali pa kushi.
Zimeshapita siku 12 tangu zaidi ya nyumba 300, zilizojengwa kwenye bonde hilo zibomolewe na kulazimisha wakazi kuhamia sehemu nyingine na baadhi kuishi juu ya vifusi.
Bomoabomoa hiyo ilisitishwa kwa siku 14, hadi Januari 5 mwakani ili kupisha wananchi waliojenga kwenye maeneo ya wazi, kwenye fukwe na mabondeni kuondoka kwa hiari yao.
Zaidi ya nyumba 8,000 zilizojengwa kwenye maeneo hayo zitakumbwa na kazi hiyo ya bomoabomoa inayofanywa kwa pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi, Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) na halmashauri za manispaa.
Akizungumza na Mwananchi, mjumbe wa shina la Kawawa (CCM) ambaye pia ni mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Erasto Mayani alisema wanafunzi wengi wanaoishi na wazazi wao juu ya vifusi hawataweza kuendelea na masomo yao baada ya kukosa makazi.
“Tunaendelea kufanya tathmini ili kuona hatma ya wanafunzi hawa wasio na hatia hata kidogo,” alisema. Baadhi ya wanafunzi waliiomba Serikali kuwasaidia wazazi wao kupata makazi, ili wafahamu shule watakazohamia tofauti na hali yao ya sasa kwenye bonde hilo.
Mmoja wa wanafunzi hao, Maua Juma anayesoma Shule ya Msingi Mkunguni, alisema tangu nyumba yao ibomolewe na vifaa vyao kuibiwa, hafahamu hatma yake na wadogo zake kuhusu shule.
“Muda mwingi mama yangu anautumia kulia tu, hata tukimuuliza tutafanyaje kuhusu shule hasemi chochote. Kwa kweli tumekata tamaa kabisa, kila siku tunalala nje na mbu wanatung’ata kupita kiasi,” alisema mwanafunzi huyo anayeinbgia darasa la saba.
“Kama si kuugua malaria, basi homa za matumbo hatutaweza kuepuka. Sula la shule itabidi tusahau kabisa.”
Maua, ambaye wadogo zake watatu wanasoma shule hiyo, alisema hawana sare wala vifaa vingine vya shule baada ya vitu vyao kuharibiwa wakati wa bomoabomoa.
Mwanafunzi mwingine wa shule ya Sekondari Msimbazi, Idrisa Jacob alisema hana uhakika wa kuendelea na masomo ikiwa watakosa eneo la kuhamia.
CHANZO:MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni