Polisi nchini Ubelgiji wamewakamata watu wawili wanaotuhumiwa kupanga mashambulio mkesha wa siku ya Mwaka Mpya mjini Brussels.
Walikamatwa kwenye misako ya polisi Jumapili na Jumatatu mjini Brussels na katika mikoa ya Flemish Brabant na Liege.Polisi walipata sare za jeshi na nyaraka za kueneza propaganda lakini hakupata silaha zozote wala vilipuzi.
Ubelgiji imekuwa katika hali ya tahadhari tangu kutokea kwa mashambulio ya 13 Novemba mjini Paris.
Wahusika kadha wa mashambulio hayo wanadaiwa kuwa na makao yao nchini Ubelgiji.
Hata hivyo, maafisa wanasema watu hao wawili waliokamatwa hawana uhusiano na mashambulio hayo ya Paris yaliyoua watu 130.
Mmoja wa waliokamatwa anashukiwa kuongoza kundi la magaidi na kuandikisha wanachama.
Washukiwa hao wanatuhumiwa kupanga mashambulio katika maeneo kadha Brussels, na dhidi ya polisi, kwa mujibu wa runinga ya taifa ya Ubelgiji RTBF.
Nyaraka za propaganda kutoka kwa kundi linalojiita Islamic State ni baadhi ya vitu vilivyonaswa na polisi.
Mwezi Novemba, shughuli muhimu zilimamishwa kwa siku nne na vyuo, shule na vituo vya uchukuzi kufungwa, maafisa wakihofia kutekelezwa kwa shambulio sawa na la Paris.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni