Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa
Jumanne Maghembe, aliyeapishwa jana kushika wadhifa huo na Rais Dk. John
Magufuli, amefunguka na kueleza sababu za kuitwa Waziri ‘mzigo’ wakati
akiwa Wizara ya Maji, akitokea Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Novemba 24,mwaka 2013, Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, akiwa kwenye ziara za
kuimarisha na kukagua Ilani ya chama hicho mkoani Ruvuma, kabla ya
kuanza kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, alikutana na malalamiko ya
wananchi juu ya uzembe wa mawaziri waliokuwa kwenye Serikali ya Rais
Jakaya Kikwete, waliowaita ‘mizigo’.
Mawaziri wengine waliotajwa kuwa mizigo
ni Dk. Shukuru Kawambwa (Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi),
Christropher Chiza (Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika) na Naibu wake
Akijibu tuhuma hizo baada ya kupenya
kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Dk. Magufuli, tofauti na watu wengi
walivyodhani kutokana kashfa hiyo, Profesa Maghembe alisema waliomtaja
kuwa ni mzigo ni majangili waliokuwa wanawinda wanyama na waandishi
waliokuwa wanaandika na kulipwa na majangili.
“Wanaosema Waziri Maghembe ni mzigo
hawajui na hawajafanya utafiti na usipofanya utafiti, huna haki ya
kuzungumza, na wafikishieni taarifa Maghembe amerudi tena,” alisema.
Alisema amejipanga kuhakikisha anapambana na ujangili nchini na kuongeza pato la taifa kupitia sekta hiyo.
Alisema atahakikisha wizara hiyo inaenda vizuri na rasilimali zilizopo zinalindwa ili zilifaidishe taifa.
“Jambo la
kwanza nitakalolifanya ni kupambana na ujangili na tunawatumia salamu
majangili wote kokote walipo, kiama chao kimefika…kwa sasa wakae
nyumbani watafute shughuli za kufanya,” alisema.
Alitaja jambo la pili atakalolifanya
katika sekta hiyo ni kuhakikisha misitu inatunzwa na kudhibiti watu wote
wanaokata miti na kuchoma mkaa.
“Tutahakikisha mkaa utakaokuwa unachomwa
ni ule wa lazima na siyo kuchoma hovyo. Hivyo tutaangalia namna ya
kurahisisha nishati zilizopo ili kupunguza matumizi ya mkaa,” alisema.
Prof. Magembe alisema jambo la tatu ni
kuhamasisha utalii na kuongeza idadi ya watalii kutoka nje kutoka
milioni 1.2 hadi kufikia milioni tatu katika kipindi cha miaka mitatu.
“Hii ni sekta muhimu na ili kuongeza
idadi ya watalii kufikia milioni mbili hadi tatu kwa kipindi cha miaka
miwili ama mitatu ijayo ni lazima kuhamasisha,”alisema.
Alisema mwaka 2007 akiwa Wizara ya
Maliasili na Utalii, katika kipindi hicho, alifanya kazi kubwa ya
kuhakikisha katika sekta ya uwindaji wanaongeza mapato ya serikali
kuanzia Dola milioni saba zilizokuwa zinapatikana hadi kufikia Dola
milioni 70 na kwa msingi huo, yeye siyo mzigo.
Alisema pia walikuwa wakifanya kazi ya
kukamata watu wanaosafirisha magogo kwenda nje ya nchi na kuongeza pato
la taifa katika sekta ya misitu.
“Nashangaa hawa wanaoniita mimi ni mzigo, ningewezaje kufanya kazi hizi,” alisema Profesa Maghembe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni