TANGAZO

TANGAZO

Jumamosi, 12 Desemba 2015

KINANA AMVAA LOWASA ARUSHA

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahmani Kinana akihutubia mkutano wa hadhara.
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amemjibu aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, aliyedai kuwa kazi nzuri anazofanya Rais John Magufuli, ni utekelezaji wa sera za vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za mgombea ubunge wa Arusha, Philemon Mollel (Monaban), uliofanyika katika kata ya Daraja Mbili jana, Kinana alisema sera ya kupambana na ufisadi ilizungumzwa katika kampeni na Dk Magufuli peke yake na si Lowassa wala kiongozi yeyote wa Ukawa.
Kinana alisema anamshangaa kiongozi huyo kwa kuwa mbali na kushindwa kuzungumza wakati wa kampeni za urais, pia hakuwa na hotuba yoyote ambayo ingeweza kukaririwa na Dk Magufuli.
Alisema Lowassa hakuweza kuzungumzia masuala yoyote ya kupambana na ufisadi kwa kuwa yeye ni mtuhumiwa na vyama vina vyounda umoja huo ndiyo vimekumbatia ufisadi kwa sasa.
Kwa mujibu wa Kinana, Lowassa alinadi sana mabadiliko kama angeweza kuingia madarakani, lakini hakufafanua ni mabadiliko yapi ambayo angeweza kuyaleta, wakati anatoka katika mfumo ule ule aliokulia kwa zaidi ya miaka 40 akiwa ndani ya CCM na Serikali yake.
“Jamani Lowassa alisema mabadiliko lakini hao wanaotaka mabadiliko wana umri wa ujana sawa na jua linalochomoza la saa mbili asubuhi, wakati yeye anayedai kuleta mabadiliko ana umri wa uzee sawa na jua linalozama la saa 12.30 jioni, si vichekesho hivyo?” Alihoji Kinana.
Alisema kutokana na ukweli huo, ndiyo maana Watanzania walipima na kuamua kumpa ushindi wa kishindo Dk Magufuli, kutokana na uadilifu wake pamoja na uwezo wake wa kuchapa kazi na kuamua kumnyima Lowassa na ndiyo maana kwa sasa anajifariji kwa kusema sera zinazotekelezwa ni za Ukawa.
Akizungumzia kazi alizoanza kuzifanya Rais Magufuli, Kinana alisema zimewakuna Watanzania wengi na kusema kuwa hiyo ndiyo kazi aliyoahidi kwao kuifanya na kwamba anaamini ataifanya kwa dhati katika kuwapigania wananchi wanyonge.
Mfumo CCM Akizungumzia madai kuwa hakuna kiongozi yeyote atakayetokana na CCM anayeweza kupambana na machafu ndani ya Serikali, kwa kuwa hilo ni suala la mfumo, Kinana alipinga na kusema si kweli.
Akifafanua alisema mfumo unaweza kubadilishwa hata na mtu mmoja kama anavyofanya Dk Magufuli, Makamu wake, Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema moja ya mambo aliyoyaondoa Magufuli katika mfumo huo, ni pamoja na kufuta safari za nje kwa viongozi akiwemo yeye binafsi, kuondoa semina, warsha, makongamano, sherehe na maadhimisho mbalimbali pamoja na posho mbalimbali na kuagiza fedha hizo kwenda katika mahitaji mengine ikiwemo hospitalini.
Akizungumzia uchaguzi wa ubunge unaotarajiwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu, Kinana aliwataka wananchi wa Jimbo la Arusha Mjini, kuachana na ushabiki wa vyama na badala yake wachague kiongozi kutokana na sifa zake na kuangalia maslahi yao na siyo ya chama wala kiongozi husika.
Alisema kwa sasa wananchi wa jimbo hilo wanapaswa kuangalia maslahi yao katika kumchagua mbunge, yakiwemo maslahi ya shule, afya, miundombinu, amani pamoja na mambo mengine mengi, badala ya kubaki kuimbiwa kuwa wanafundishwa kuiwajibisha Serikali huku wakibaki katika lindi la umasikini, ukosefu wa amani na maandamano kila kukicha.
Taarifa ya NEC
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva akizungumzia uchaguzi huo unaofanyika kesho, amewasihi viongozi wa vyama vya siasa kutoingilia shughuli za tume hiyo, ili waipe nafasi ya kusimamia uchaguzi na kutangaza matokeo kwa uhuru na haki.
Alisema Jumapili hii kutafanyika uchaguzi katika majimbo mawili ambayo ni Handeni na Arusha Mjini, ambapo kwa Mkoa wa Arusha, idadi ya waliojiandikisha ni 317,814 na vifaa vyote vimeshakamilika.
Jaji Lubuva alisisitiza viongozi wa vyama vya siasa na viongozi mbalimbali kutoingilia kazi za NEC, huku akisema daftari litakalotumika ni lile lile la Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba mwaka huu. Aliwataka wasimamizi wa uchaguzi na mawakala, wahakikishe hakuna mtu atakayepiga kura zaidi ya mara moja.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini, alisema vituo vyote vya kupigia kura ni 721 na aliwaomba wapiga kura wajitokeze kupiga kura na kurudi nyumbani kwa sababu hakuna haja ya vurugu wakati kuna maisha baada ya uchaguzi.
Alisema katika uchaguzi huo wagombea wako watano ambao ni Godbless Lema (Chadema), Philemon Mollel (CCM), Bibi Navoi Mollel (ACT Wazalendo), Hamisi Zuberi (CUF) na Rashidi Mkama (NRA).
CHANZO:HABARI LEO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni