Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk Edmund Kayombo akizungumza na wandishi wa habari kuhusu kutotambuliwa kwa mkutano wa waganga wa tiba mbadala uliofanyika juzi.
PICHA NA :MWANANCHI COMMUNICATION.
Dar
es Salaam. Serikali imesema ina taarifa za kuingizwa kwa mashine za
kuchukulia vipimo bila ya kusajiliwa na kusisitiza kuwa itaweka bayana
msimamo wake baada ya siku 14 ilizotoa kwa matabibu wa tiba mbadala
kuwasilisha taarifa za huduma zao.
Waziri
wa Afya, Ummy Mwalimu pia amesema jana kuwa Serikali itaendelea kuzuia
matangazo ya tiba asili na mbadala yasiyokuwa na kibali ili kudhibiti
taarifa zinazoweza kusababisha madhara kwa umma.
Tamko
hilo la Serikali linatokana na mvutano ulioibuka baada ya Naibu Waziri
wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla kupiga marufuku matangazo ya waganga wa
tiba mbadala ambao wamekuwa wakinunua muda kwenye vituo vya redio na
televisheni na kupigia debe kliniki zao kuwa zinatimu magonjwa sugu.
Uamuzi
huo wa Dk Kigwangalla ulipingwa vikali na waganga hao waliokutana
jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, wakidai kuwa sheria inawaruhusu
kujitangaza.
Mvutano
huo umeibuka wakati gazeti la The Citizen likifichua kifaa cha
kielektroniki ambacho kimekuwa kikitumiwa na baadhi ya waganga wa tiba
mbadala kufanyia uchunguzi wagonjwa na kutoa majibu yenye taarifa nyingi
za mwili katika muda usiozidi dakika mbili.
Jana Waziri Mwalimu alisema kumekuwapo na uingizaji wa vifaa tiba hivyo bila ya kuvisajili na kwamba Serikali itachukua hatua.
Alisema
sheria inataka kila kifaa cha tiba mbadala kinachoingizwa nchini,
kisajiliwe kabla ya kuanza kutumika. “Jana nimemsikia mtu anatibu
matatizo yote ya uzazi, nikajiuliza inawezekana vipi,” alisema Waziri
Mwalimu.
Moja
ya vifaa hivyo ni Quantum Magnetic Analyser, ambayo watengenezaji
wanasema inaweza kuchukua taarifa nyingi za mwili ndani ya dakika mbili
na kutoa majibu, ambayo hutumiwa na waganga hao kumshawishi mgonjwa kuwa
ana matatizo sugu ya kiafya na hivyo anahitaji tiba mbadala.
Uchunguzi
unaofanywa na kifaa hicho ambao haumsababishii mgonjwa maumivu wakati
wa kuchunguzwa, unatiliwa shaka na wataalamu mbalimbali kuhusu usahihi
wa taarifa zake.
Kuhusu
matangazo ya kwenye televisheni na redio, alisema Serikali haina ugomvi
na waganga wa tiba mbadala, akisisitiza kuwa iko tayari kukutana nao
kujadili tamko lake kuhusu matangazo yao kwa lengo la kuboresha huduma
kwa wateja wao.
“Naomba
niweke wazi kwamba tiba asili na mbadala ni sehemu ya utoaji wa huduma
za afya katika nchi yetu. Tunazitambua na kuzithamini,” alisema.
“Lakini tamko la wizara linabaki kuwa la Serikali kwa sababu kuna baadhi ya watoa tiba kwa kiasi kikubwa wanakiuka taratibu.”
Alisema
licha ya zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania nchini kutegemea tiba hizo,
kuna changamoto katika utoaji wake. Alisema sheria na kanuni zinataka
tabibu ajisajili, kusajili kituo chake cha kutoa huduma au taarifa,
dawa, vifaa tiba anavyovitumia na matangazo.
Alisema
kanuni ya 10 ya sheria hiyo inasema hakuna tangazo lolote
litakalotolewa kuhamasisha tiba hizo kwenda kwa umma isipokuwa
limeidhinishwa na baraza hilo, hivyo tamko la wizara ni sahihi.
Baraza lalonga
Kwa
upande wake, Baraza la Tiba Asili na Mbadala liliunga mkono tamko hilo
la kuzuia matangazo na kuagiza anayetaka kutangaza huduma yake, lazima
apitie kwao ili kupata kibali.
Kaimu
mkurugenzi wake, Mboni Bakari alisema licha ya kutolewa vibali kwa
baadhi ya matabibu wanaotoa matangazo yao kupitia vyombo vya habari,
wamekuwa wakikiuka makubaliano wanayopewa.
Mwenyekiti
wa baraza hilo, Dk Edmund Kayombo alisema: “Tunaomba matabibu wawe
watulivu na shirikisho na baraza kwa kushirikiana na wizara ya afya kwa
ujumla tunaendelea na vikao na wiki hii tunatarajia kutoa tamko. Kikubwa
watupe ushirikiano na kuonyesha utii wa sheria.”
Shirikisho lanena
Mwenyekiti
wa Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili na Mbadala Tanzania
(Shivyatiata), Abdalrahman Lutenga alisema agizo la Serikali ni la
kisheria na siyo jipya kwa sababu sheria inaeleza matangazo yote lazima
yapitie baraza hilo kuhakikiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni