Morogoro.
Wakulima wadogo wilayani Kilosa wameonekana kukosa ufahamu wa sheria za
ardhi, jambo linalowafanya kushindwa kufuatilia kwa makini masuala ya
ardhi pale inapotokea migogoro katika maeneo yao.
Mkuu
wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Miradi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Dk Adam Nyaruhuma alisema hayo katika mkutano wa
wakulima wadogo wilayani humo, juu ya utafiti kuhusu migogoro ya ardhi
alioufanya na kugundua upungufu uliopo.
Dk
Nyaruhuma alisema katika utafiti wake aligundua upungufu uliojitokeza
ukiwamo utoaji elimu kwa wakulima kutoka kwa wataalamu mbalimbali.
Alitaja
upungufu mwingine kuwa ni wananchi kutokuwa na uelewa juu ya Sheria ya
Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya
mwaka 1999 pamoja na Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 ambayo iliboreshwa
mwaka 1997.
Mtafiti
huyo aliiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji
juu ya masuala ya ardhi ambayo yamekuwa yakisababisha kuwapo kwa
migogoro ya mara kwa mara wilayani Kilosa.
Pia,
alisema kutokana na uelewa huo wa wananchi, hasa vijijini ifike wakati
kila mwananchi mwenye kipande cha ardhi kipewe hati ya umiliki ili
kupunguza au kuondoa kabisa migogoro inayojitokeza.
“Kutokana
na kuwapo kwa migogoro baadhi ya upungufu wa sheria unaruhusu vijiji
kimoja hadi vitatu kukaa pamoja na kumiliki ardhi kwa mkataba wa pamoja.
Ni vyema Serikali ikaendelea kufanya marekebisho ya mara kwa mara,”
alisema.
Dk
Nyaruhuma alisema sheria hairuhusu kufanya shughuli za kilimo au
ufugaji katika vijiji bila kuwa na cheti cha kimila cha umiliki wa
ardhi.
Wakizungumza
katika mkutano huo, wakulima Andrew Kikule na Sara Kalunde walisema
endapo Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji,
migogoro katika maeneo yao itamalizika. “Tumekuwa na migogoro katika
wilaya yetu kutokana na kutokuwa na mpangilio wa kueleweka na kila
upande unajiona kuwa na haki ya kumiliki,” alisema Kikule.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni